Kwa muda mrefu, nilidhani mwisho mwema wa hadithi ya mapenzi ulikuwa wazi: mwanamke huyo angenichagua, umbali kati yetu ungeisha, na hatimaye tungeishi pamoja.
Nilikuwa nimemfahamu kwa miongo kadhaa. Urafiki wetu ulivuka miji, mashamba na miaka mingi ya kuandikiana barua, hadi hatimaye niliposafiri kwenda kumtembelea nchini Kolombia
Nilikuwa na matumaini mengi sana katika safari hiyo, kiasi kwamba hata mambo madogo niliyoyashuhudia, ambayo kwake yaliyoonekana ya kawaida niliyaona kama ushahidi wa maisha ya baadaye ambayo hatukuwa tumekubaliana kuyajenga pamoja.
Nilipofika, tayari alikuwa na maisha yake, familia, majukumu, kazi na watu waliokuwa muhimu kwake.
Nilifika nikiwa na mapenzi na nia njema, lakini pia nikiwa na mazoea ya kupenda kutatua kila tatizo litakalojitokeza kwake. Nilifikiri kwamba kumsaidia kungenifanya kuwa karibu naye zaidi.
Nilichelewa kutambua kwamba; katika kujaribu kutoa msaada, unaweza kumuwekea mwingine presha kubwa bila hata kukusudia.
Majuzi tu, nilikua nawaza mwisho tofauti kabisa wa hadithi yetu, kama vile tungo na simulizi nyingi; mara nyingi mwisho huwa unafanya watu kukutana tena, kujifunza kuishi pamoja, kisha kufunga ndoa. Ndoa hiyo haikufanyika kwangu katika maisha halisi. Ilikuwa ni sawa na mimi kuweka matamanio yangu katika kurasa za simulizi na si matakwa ama maamuzi yake.
Niliandika mwisho ambao ningeutamani: kukutana tena uwanja wa ndege, maua, na harusi katika bustani. Kisha nikajaribu kuwazia, je, mwisho huo niutamanio ni mwisho ambao mwanamke huyo angeuhitaji pia?
Hatimaye, harusi ikaacha kuwa tukio muhimu katika simulizi, badala yake, nilitumbukia katika mawazo fulani ya mabishano ya wapendanao wawili kuhusu tangazo la nyumba inayouzwa;
Mwanaume aliona tangazo la uuzwaji wa nyumba nzuri, yenye bustani na nafasi kubwa, kisha akaleta na kuweka tangazo hilo karibu na kikombe cha kahawa cha mwanamke wake. Akidhani ameweka maisha yao ya baadaye mezani, alidhani alikuwa akiweka mezani picha ya maisha yao ya baadaye. Lakini mwanamke huyo hakuwa amemwomba amtafutie maisha hayo.
Katika mawazo yangu hayo ya kubuni kuhusu tukio hilo, nawaza inatokea mwanamke anamwambia mwanamume kuwa: ukarimu ni bora bila hata yeye kuchagua, lakini, uhalisia ni kwamba, maneno hayo yalikuwa yangu, si yake, na nilihisi ukweli wa msemo huo ni kwa tabia zangu mwenyewe.
Katika maisha halisi, nilikuwa nimewahi kutoa mapendekezo ya namna hiyo: nyumba, mashamba, matembezi na mipango. Kila pendekezo lilibeba tumaini lakini pia kila moja lilikuja na hatari yake pia.
Ningeweza hata kutafsiri shauku ya heshima kama ukubali, au kuona kusita kwake kama kupotea kwa jambo ambalo halikuwa limeahidiwa.
Somo la kwanza nililopata kutokana na zoezi hilo ni kwamba: mpango mzuri si lazima uwe mpango wa watu wawili.
Tunapomjali sana mtu, tunaweza kujali zaidi maisha ya baadaye tutakayompatia, kiasi cha kutumia muda mrefu sana kuwazia furaha itakayopatikana katika maisha hayo huku tukasahau kuuliza kama mtu huyo anahitaji kuyaishi malengo na maono hayo pia.
Suluhisho si kuacha kuota ndoto njema kwa ajili yenu nyote bali ni kumshirikisha na kumsikiliza mwenzako badala ya kumfanya ajisikie kwamba lazima akubali ndoto uliyomuwazia.
Badala ya kusema, “Nimepata nyumba inayotufaa,” ninaweza kusema, “Niliona kitu kilichonikumbusha wewe. Ungependa kukiona?” Swali la pili linaruhusu jibu la kweli, hata likiwa “Hapana” au “Si sasa.”
Jibu likinivunja moyo, ninaweza kukubali hisia hiyo bila kuigeuza kuwa deni atakalolilipa mtu mwingine.
Hapo ndipo nilipopata somo la pili: hatuwezi kutumia wema kununua uhakika.
Mara nyingi nimetaka kutatua matatizo, kupanga mambo ya kila siku na kuwa mtu mwenye msaada. Hakuna ubaya kumpelekea mtu chakula, kumpa usafiri au kumsikiliza wakati maisha yakiwa magumu. Tatizo huanza ninapotarajia kwamba matendo hayo yatanifanya mtu nisiyekwepeka maishani mwake.
Kulazimisha kuhitajika si msingi imara katika mapenzi. Mtu mwenye uwezo anaweza asihitaji ushauri wetu. Mzazi mwenye majukumu mengi anaweza kuthamini msaada wetu lakini bado akachagua maisha ambayo hayatuhusishi kwa namna tunayotamani.
Sasa, kabla sijatoa msaada siku hizi, huwa najiuliza kwanza: “Je, ningeendelea kutoa msaada huu kama nisingeona hatua hata hatua moja kuelekea mwisho ninaoutamani?”
Jibu likiwa hapana, huenda ninajificha nyuma ya zawadi ili kuwasilisha ombi ambalo sijasema wazi. Inakuwa bora zaidi kuuliza moja kwa moja ninachokihitaji: muda wa kuwa pamoja, uhakika na ufafanuzi wa wazi kuhusu uhusiano wetu.
Somo la tatu lilitokana na tukio jingine nililowazia. Mwanamke anarudi Kolombia kuendelea na maisha yake. Hata mwanamume akimkumbuka kiasi, hatogeuza umbali wao kama kipimo cha mara ngapi anapigiwa simu au uharaka wa kujibiwa meseji.
Zamani, nilikuwa nikichukulia kusubiri kama kipimo cha upendo. Ujumbe ulipofika, niliusoma kwa makini. Ujumbe usipofika, niliusoma ukimya huo kwa umakini zaidi.
Ratiba ya mtu mwingine si kipimo halisi cha thamani yetu. Upendo hauwezi kuwa huru ikiwa maelezo yatahitajika mara zote mtu asipokuwepo, na kila uamuzi wa binafsi kutafsiriwa kama kukataliwa.
Katika hadithi ya kubuni, hatimaye mwanamke huyo anarudi kwa sababu yeye mwenyewe anataka kurudi, si kwa sababu mwanaume amemshawishi afanye hivyo. Tofauti hiyo ilinivutia zaidi kuliko harusi.
Nilianza kuelewa kwamba ahadi ya kuwa pamoja katika uhusiano kuna maana hasa kwa sababu hakuna anayelazimishwa kufanya hivyo. Tunaweza kuomba kujenga maisha pamoja, lakini hatuwezi kuruhusu hamu yetu kubwa ya kuwa na mtu ichukue nafasi ya maamuzi yake.
Somo hili linafaa hata katika mahusiano ambayo tayari yana msingi imara. Mwenza anahitaji nafasi ya kuwa na marafiki, kazi, majukumu ya familia na maoni tofauti. Watu wawili wanaweza kutokubaliana kuhusu safari moja au nyumba bila kuchukulia tofauti hiyo kama kipimo cha upendo wao.
Inasaidia sana kufanya mwaliko uwe mdogo na wa wazi. “Ungependa niandamane nawe katika safari hii?” ni bora kuliko “Sisi husafiri pamoja kila wakati.” “Tunaweza kuzungumza kuhusu namna ya kuishi?” ni bora kuliko kufika na mpango ambao tayari umekamilika bila kushirikisha mwenzako.
Na mtu anaposema hapana, tunaweza kujifunza kubaki wenye fadhili hata tunapohisi kuvunjika moyo. Huo si udhaifu wala kukubali kila jambo bila kuuliza. Ni kuwajibika kwa hisia zetu wenyewe.
Hapa kuna zoezi ninalotumia ninapohisi kwamba ninakimbilia mbele mno. Ninaandika maisha ya baadaye ninayoyawazia pamoja na mtu mwingine. Kisha, chini yake, ninaandika majibu mafupi kwa maswali matatu: Tumekubaliana nini hasa? Ni mambo gani ninayodhani tu bila kuyathibitisha? Ninaweza kuuliza nini bila kumwekea shinikizo?
Baada ya hapo, ninachagua jambo moja la kawaida ambalo halihitaji ahadi yoyote ya matokeo kama vile: kuandaa chakula cha jioni, kwenda matembezini, kukamilisha kazi zangu mwenyewe au kumtembelea rafiki. Lengo si kuzima matumaini. Ni kujikumbusha kwamba maisha ninayoishi sasa nayo yanastahili kupewa umakini, hata wakati ujao unapokuwa bado hauna uhakika.
Kadiri nilivyoendelea kuwazia ndoa hiyo, niligundua jambo jingine. Harusi haiondoi magonjwa, mahangaiko, matatizo ya kifedha wala hitaji la kuomba msamaha. Ahadi ya ndoa ingekuwa na maana ndogo ikiwa watu wawili wasingeweza kuendelea kuwa wao wenyewe baada ya kufunga ndoa.
Tukio lililobaki akilini mwangu halikuwa la viapo vya harusi. Lilikuwa la watu wawili wakipakia sanduku la safari. Walikuwa wametofautiana, lakini sasa walikuwa wakikunja mashati pamoja, bila ustadi wowote na huku wakicheka. Mmoja wao bado alikuwa anaondoka. Lakini upendo kati yao bado ulikuwepo.
Tukio hilo lilikuwa la kubuni. Lakini uelewa nilioipata kupitia tukio hilo ulikuwa wa kweli.
Zamani, nilidhani nilihitaji mtu anichague ili maisha yangu yawe kamili. Sasa ninajifunza kujenga maisha ambayo mtu mwingine anaweza kuingia kwa hiari, kubaki kwa hiari, na kusema ukweli bila kuogopa kwamba kufanya hivyo kutamnyima wema wangu.
Ikiwa siku moja upendo utazaa ndoa, natumaini itakuwa kwa sababu watu wawili wanaendelea kuchaguana. Ikiwa hautakuwa ndoa, upendo na kujali walivyoshirikiana bado vinaweza kuwa vilikuwa vya kweli.
Labda huo ndio mwisho wenye furaha ulio mgumu zaidi: si kupata jibu tulilotamani, bali kuwa mtu anayeweza kusikia jibu la kweli na kuendelea kupenda bila kumfunga mwingine.